KARIBUNI SA

Sunday, March 28, 2010

JAKAYA ATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI


Rais Jakaya Kikwete, amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi, kutokana na vifo vya watu 10 waliopoteza maisha kwa ajali ya barabarani.

Ajali hiyo ilitokea juzi eneo la Kibamba, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam baada ya lori kubwa la mafuta lenye tela, kugongana na basi dogo la abiria aina ya Hiace na hatimaye kulilalia na kusababisha watu wote waliokuwemo kwenye basi hilo kufariki dunia.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, jijini Dar es Salaam jana ilisema kupitia kwa Lukuvi, Rais Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa wote walipoteza ndugu zao katika ajali hiyo mbaya.

“Kupitia kwako, ninatuma salamu za rambirambi kwa watu wote waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika ajali hiyo mbaya,” alisema.

Aliongeza: “Ninaelewa fika ni kwa kiasi gani hivi sasa ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu wanaelemewa na huzuni kubwa na majonzi baada ya kuwapoteza wapendwa wao.”

Taarifa ilisema Rais Kikwete amewaomba wafiwa wote wawe na moyo wa uvumilivu na ujasiri wakati huu mgumu wa maombolezo ya vifo vya ndugu, jamaa na marafiki zao na amemuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, azilaze roho za marehemu wote mahali pema peponi.

Katika salamu zake hizo, Rais Kikwete, amezisisitizia mamlaka zinazohusika na Sheria ya Usalama Barabarani, kuisimamia kikamilifu sheria hiyo ili Taifa lisiendelee kupoteza watu wake kutokana na kukiukwa kwa sheria hiyo.

No comments:

Post a Comment