Dodoma
WANAFUNZI zaidi ya 400 waliofukuzwa chuo kikuu cha dodoma hivi karibuni kwa kuandamana kudai fedha za kwenda mafunzo kwa vitendo watarejeshwa kwa mafungu huku vinara wa maandamano hayo wakikabiliwa na hatari ya kufukuzwa moja kwa moja ili iwe fundisho kwa wanafunzi wengine wanaogoma.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (udom), Prof Idris Kikula pichani alisema juzi chuoni hapo kuwa, uamuzi huo ulifikiwa jana na Kamati ya Utendaji ya Baraza la uongozi la chuo hicho lililokutana kujadili matatizo yaliyosababisha wanafunzi hao wakagoma na kuandamana licha ya Serikali kutoa fedha za mafunzo kwa vitendo.
“Baada ya Serikali kukubali kutoa fedha za wanafunzi kwenda mafunzo kwa vitendo, nilienda saa sita usiku kuwaambia kuwa serikali imetoa fedha na hivyo hawakuwa na sababu ya kuandamana kesho yake kama walivyokuwa wamepanga lakini kwa kuwa walikuwa na ajenda nyingine zaidi ya fedha, walikataa na kuandamana. Kutokana na hali hiyo, Kamati ya Utendaji iliyokutana leo(jana) imeamua kukubaliana na uamuzi wa chuo kuwafukuza na kisha kuweka masharti ya jinsi ya kuwarudisha wale ambao hawataonekana kuhusika moja kwa moja na chanzo cha maandamano hayo, |Profesa Kikula alisema ofisini kwake.
Alisema kamati hiyo imeamua kuidhinisha mapendekezo na maamuzi ya Kamati ya Ushauri ya Udom iliyokutana Juni 13 na Juni 14 mwaka huu ya kuwafukuza wanafunzi wote wa Chuo ya Sayansi za asili na hesabu (SNM) na Chuo cha Sanaa na Sayansi za Jamii (COHSS) wapatao 400 ili uchunguzi kubaini wahusika ufanyike na adhabu stahili zichukuliwe kwa watakaobainika kuwa chanzo cha maandamanano hayo au kuwalazimisha wengine kuandamana isivyo halali.
Proff. Kikula alisema Kamati ya Utendaji iliyokutana jana iliidhinisha mapendekezo ya Kamati ya ushauri iliyopendekeza pamoja na mambo mengine kuwafukuza wanafunzi wote wa shahada ya kwanza wa COHSS, kuwachukulia hatua za kinidhamu, wanafunzi wote waliohusika na maandamano hayo na kwamba wanafunzi waliofukuzwa warudishwe chuoni kwa utaratibu maalum utakaotangazwa baada ya uchunguzi kubaini wahusika wakuu kufanyika.
Makamu Mkuu huyo wa chuo aliutaja utaratibu wa kuwarejesha chuoni wanafunzi kuwa ni pamoja na wanafunzi wa mwaka wa tatu wa shahada ya kwanza kurejeshwa chuoni kwa ajili ya kufanya mitihani yao katika siku itakayotangazwa baada ya mamlaka ya nidhamu kufanya uchunguzi wa kina dhidi yao.
Alisema wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wa pili ambao hawataonekana na makosa pia wataruhusiwa kurejea chuoni katika siku itakayotangazwa baada ya mamlaka ya nidhamu ya Udom kuwachunguza na kuwabaini wale ambao hawakuhusika katika maandamano hayo yanayodaiwa kuchagizwa na vyama vya upinzani.
Profesa kikula alisema mbali ya wanafunzi wa shahada za SNM na CoHSS, Kamati ya Utendaji ya Baraza la uongozi la Udom pia ilikiubaliana na pendekezo la kuwarejesha pia wanafunzi wa mwaka wa pili wa shahada ya kwanza ya uhusiano wa kimataifa (IR) waliofukuzwa Juni 14 lakini baada ya uchunguzi dhidi yao.
Kuhusu wanafunzi 24 wanaodaiwa kuwa vinara wa maandamano hayo kutoka SNM ambao wanadaiwa kuongoza mgomo wa kuingia darasani na kuwalazimisha wanafunzi wenzao wajiunge na mgomo na maandamano hayo, profesa alisema hatma yao itaamuliwa baada ya uchunguzi wa kina wa mamlaka ya nidhamu ya UDom.
Alisema hatma ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza wote wanaochukua shahada ya kwanza ya Sayansi ya takwimu (Bsc Statistics) na 41 wanaochukua shahada ya kwanza ya sayansi katika hesabu (Bsc in mathematics) ambao waliandika barua na kuzisaini mara mbili kwa hiari yao nao waondoke chuoni kupinga wenzao kutimuliwa nayo pia itaamuliwa na mamlaka ya nidhamu ya udom baada ya uchunguzi wa kina kufanyika kupata adhabu inayowastahili.
Pia alisema wanafunzi 36 wa shahada ya kwanza ya sayansi ya hesabu (bsc. Mathematics) waliokataa kwa kuandika barua kushiriki katika mgomo na maandamano hayo licha ya kulazimishwa na wenzao Kamati ya Utendaji ya Baraza la uongozi la chuo imeamua hao waendelee na masomo yao.
Profesa alisema tarehe za wanafunzi watakaorejeshwa kurudi chuoni zitatangazwa na mamlaka mambo yatakapokuwa tayari lakini akaonya kuwa safari hii hawana mzaha kwani watakaobainika kujihusisha na maandamano hayo na kuwa vinara hawatarejeshwa kabisa chuoni ili iwe fundisho kwa wengine.
Alisedma hayo huku kukiwa na habari kuwa, wanafunzi waliogoma na kuandamana baadhi yao waliripotiwa kuwa kabla ya kutimuliwa, walikuwa wamekwenda mjini dodoma kuchukua mafuta ya petroli ili kuja k,ulipua majengo ya chuo kikuu hicho kwa lengo la kuitia hasara serikali iliyokijenga kwa mabilioni ya fedha.
Hatua ya kamati ya utendaji ya baraza la uongozi la chuo kutaka kuwarejesha wanafunzi wasio na hatia na pia kuwaadhibu waliokuwa vinara wa maandamano imechukuliwa siku chache baada ya wabunge kuiomba serikali iwasamehe na kuwarejesha chuoni kufuatia baadhi yao hasa wanafunzi wa kike kudaiwa kudhalilika baada ya kufukuzwa ghafla na kukosa mahali pa kwenda kujihifadhi na hivyo kujikuta wakizurula mitaa mbalimbali ya mji wa dodomausiku.
CHANZO; Jambo Leo
No comments:
Post a Comment