KARIBUNI SA

Friday, April 9, 2010

POLISI WAWAPIGA RAIA RISASI

Polisi wilayani Rorya mkoa wa Mara, wamefyatua risasi za moto katikati ya raia na kuua watu wawili na kuwajeruhi wengine tisa.

Idadi ya vifo inaweza kuongezeka kwani wakati tunakwenda mitamboni habari zilionyesha kwamba baadhi ya majeruhi walikuwa na hali mbaya.

Waliokufa katika tukio hilo, wamejulikana kuwa ni Iranda Matoka (26) na Abbas Adek (23).

Aidha, majeruhi walitajwa kwa majina ya Wandiba Nyamkondya (26), Julius Nduku (26), Aziz Mganga (18), Sanga Matiko (32), Isiro Magesa (38), Ezekiel Robert (15), Ramadhani Magige (32), Musoba Rhobhi (32) na Leonard Kahanga.

Tukio hilo lilitokea jana, wakati askari hao walipokabiliana na wakazi wa kijiji cha Moharango, walioandamana kwenda kituo cha polisi Utegi, wakitaka kuachiwa huru kwa wazee wanne wa mila.

Wazee hao waliojulikana kwa majina ya Kahanga Mwando, Odila Runyola, Saba Kahanga na Wasaga Mganga, walikamatwa kwa madai ya kutishia kumroga na kumuua mkazi wa kijiji hicho, Joseph Ngondi.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa Nipashe, madai ya kumroga na kumuua Ngondi, yalitokana na hatua ya mwanakijiji huyo kufyeka mlima Nyabigiga, unaosadikiwa kutumika kwa masuala ya tambiko.

Watu walioshuhudia tukio hilo, waliliambia Nipashe kuwa baada ya wazee hao kukamatwa na kuwekwa ndani juzi, wanakijiji hao waliandama kwenda kituoni hapo kwa lengo linalodhaniwa kushinikiza kuachiwa kwa wazee wa kijiji, ndipo walipokabiliana na polisi waliokuwa na silaha zenye risasi za moto.

``Tulisikia milio ya risasi na baadaye vilio huku watu wakikimbia hovyo,`` mmoja wa mashuhuda ambaye jina lake halikupatikana, alisema.

Miili ya watu waliokufa na majeruhi ilipelekwa katika hospitali ya wilaya ya Tarime.

Majeruhi katika tukio hilo, miongoni mwao wakiwa katika hali mbaya, walijeruhiwa mikononi, miguuni, mgongoni na mapajani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Liberatus Barlow, hakupatikana jana kuzungumzia tukio hilo.

SOURCE: Nipashe

No comments:

Post a Comment