Muonekano mpya wa facebook, timeline ikionekana eneo kulia chini kwenye picha. |
Facebook ikiwa ni nyumba ya online kwa mamilioni ya watu duniani, hivyo mabadiliiko yanayotokea kwenye facebook ni dhahiri yanaathiri wengi wetu. Katika siku za karibuni Facebook wamekuja na kitu kipya ambacho wenyewe wanakiitaTimeline, hii Timeline ni mpangilio mpya wa kurasa za facebook ambao unamuwezesha mtumiaji kupanga picha, matukio n.k kulingana na muda husika.
Katika Timeline (Kalenda ya matukio), utaweza kupanga taarifa zako kwa mtindo wa kipekee zaidi huku ukimpa nafasi mtembeleaji kuzipitia kwa haraka zaidi. Kama utaangalia picha ya hapo juu, utaona kwenye timeline yangu mtu akija mara ya kwanza ataona marafiki, picha na mengine mengi. Siyo hayo tu, kwa kutumia Timeline mtu anaweza kuangalia matukio yako toka siku ya kwanza uliyojiunga na facebook.
Katika siku zilizopita Timeline ilikuwa ni kwa wanaohitaji, ila kuanzia tarehe moja mwezi wa pili Timeline itakuwa ni lazima, utake usitake ni lazima utumie au kwa lugha ya kiufundi tunaweza iita default. Hivyo usishangae kuona mabadiliko kwenye kurasa yako.
Kitu ambacho kimenivuta kuandika hii makala ni kuwa, ingawa Timeline ni nzuri na ya kuvutia, ila Facebook inaonekana wanazidi kufanya mambo kuwa magumu, ni dhahiri kuwa kufanikiwa kwa facebook kumekuja kutokana na urahisi wa utumiaji. Hivyo kufanya mambo kuwa magumu kutawafanya watu wengi kuikimbia au kushindwa kuifungua hususan wale walio kwenye mgao wa bandwith (internet zilizo taratibu mno). Kuna siku niliwahi kuona mpachiko wa rafiki yangu ambaye ni mtumiaji mzuri mno wa facebook, yeye alikuwa akilalamika kwa kusema nani amesema tunataka hii Timeline?
Kitu kingine kikubwa ambacho kinaniumiza kichwa ni privacy, facebook wenyewe mara kibao wamekiri kuwa privacy ni moja ya vitu vinavyowaumiza kichwa, kwenye facebook ya sasa mtu anaweza kuona matukio yako ndani ya wiki hadi mwezi, ila sasa kwenye hii Timeline mtu anaona tukio tangu siku ya kwanza uliyojiunga facebook, sasa huku si kuwaumbua watu? Chukulia mfano kwa wale wenzangu na mimi wazee wa kuongopa, huu si ndio mwanzo wa kukamatwa? Hivyo basi kwa kuweka Timeline kuwa default kutawatatiza wengi. Habari njema ni kuwa kuanzia sasa unaweza kuanza kufuta matukio kadhaa usiyopenda kuwaonesha watu hadi hapo Januari 31.
Je wewe unalionaje hili?
Chanzo UGHAIBUNI.COM