Ndugu watanzania zimebaki siku chache tuu kufikia tarehe 31 octoba 2010, ambapo wananchi wote wenye sifa ya kupiga kura watakuwa wakichagua viongozi wao ambao ni madiwani, wabunge na rais nchi nzima. Kila mwananchi aliyetimiza umri wa miaka 18 anahaki ya kupiga kura kufuatana na ibara ya 21 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Katika kipindi hiki nimekuwa nikifuatilia kampeni za wagombea na sera zao kutoka vyama mbalimbali, kusema kweli kuna tofauti kubwa na chaguzi za nyuma zilizotangulia. Kwa sasa watu wameonyesha mwamko mkubwa na mabadiliko ya kutaka kufuatilia kwa kina sera za wagombea na ilani za vyama vyao.
Ila kwa hali isiyo ya kawaida bado kuna wananchi wanaimani potofu kwamba hawatapiga kura kwa sababu kura yao moja haiwezi kubadilisha matokeo. Kwa kweli uamuzi huu unaofanywa na raia hauitaki mema nchi yetu ya Tanzania.Kuna msemo mmoja wa kiingereza unaosema ‘Try and fail than fail to try’ unamaana ni bora ujaribu na ushindwe kuliko ushindwe kujaribu.
Mimi ninapenda kusisitiza kwamba kura yako moja inaweza kuleta tofauti kubwa sana kwenye matokeo na pia tutambue kwamba tunapaswa kutumia nafasi yetu ya kikatiba kuchagua viongozi watakaotutumikia kwa kipindi kingine cha miaka mitano ijayo (2010 – 2015).
Ninaweza kukupa mfano dhahiri ambapo ulitokea kwenye moja ya uchaguzi mkuu wa rais katika nchi ya Marekani mwaka 1876. Uchaguzi huu ulihusisha wagombea wawili, mmoja kutoka chama cha Democratic ambaye alijulikana kwa jina la Samwel J. Tilden, na kutoka chama cha Republican aliyejulikana kama Rutherford B.Hayes.
Hayes alifanikiwa kushinda na kuwa rais wa Marekani kwa kumzidi mgombea mwenzake Tilden kwa kura moja tu. kwa hiyo unaweza kuona kwa jinsi gani kura moja inavyoweza kuleta mabadiliko, hasa katika nchi kama ya kwetu ambapo katiba inatambua mgombea kushinda kwa tofauti yoyote ya kura
Jamani wananchi wote wa Tanzania hasa vijana tujitokeze kwa wingi katika vituo vyetu vya kupigia kura siku jumapili ya tarehe 31 octoba 2010, ili tuweze kuchagua viongozi bora na si bora viongozi.
.